Macron na Rouhani wakutana

0
937

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amekutana na Rais Hassan Rouhani wa Iran kwa mara ya pili, wakiwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini New York nchini Marekani.

Macron amemuomba na kumsisitiza Rouhani, kukutana na Rais Donald Trump wa Marekani ili kumaliza mvutano wa muda mrefu kati ya Mataifa hayo mawili, ambayo kwa nyakati tofuati yametishiana kushambuliana.

Rais huyo wa Ufaransa amesisitiza kuwa, njia rahisi ya kumaliza mgogoro na mvutano kati ya Mataifa hayo mawili ni kwa viongozi wake kukutana na kufanya mazungumzo ya amani.

Mgogoro kati ya Marekani na Iran ulifukuta baada ya kutokea mashambulio ya ndege zisizokuwa na rubani katika visima vya mafuta nchini Saudi Arabia, na Marekani kuishutumu Iran kuwa imehusika, jambo ambalo nchi hiyo imekuwa ikilikanusha.

Licha ya Wapiganaji wa kikundi cha Houthi cha nchini Yemen kudai kuhusika na shambulio hilo, Marekani imesema kuwa haiamini kuwa Wapiganaji hao wana uwezo mkubwa kivita wa kufanya mashambulio ya kitaalamu kiasi hicho.