Baraza la Mawaziri kufuta mapori tengefu 12

0
229

Serikali imeridhia kufuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa Ekari 707,659.94, ambayo yamepoteza sifa na imeamua yagawiwe kwa Wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na ufugaji.

Uamuzi huo umefikiwa hii leo kweye kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam.

Akitoa taarifa mara baada ya kikao hicho, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Mawaziri wa kisekta wakiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, – William Lukuvi wamechambua na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi nchini iliyowasilishwa katika kikao hicho cha Baraza la Mawaziri.

“Mawaziri walichambua na kubaini kuwa vijiji vyenye migogoro ni 975 na siyo 366 kama ilivyotangazwa awali, Baraza limeamua kwamba vijiji 920 vitabaki ndani ya hifadhi, mipaka irejewe upya, vipatiwe vyeti vya ardhi vya kijiji pamoja na kupangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi, orodha ya vijiji hivyo itatangazwa baadaye”, amesema Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa, Serikali imeridhia Misitu ya Hifadhi saba yenye ukubwa wa Ekari 46,715 iliyopoteza sifa itolewe kwa Wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na ufugaji ili kuwaondolea kero za uhaba wa ardhi.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali imeridhia kumega hifadhi za misitu 14 kwa ajili ya kilimo na ufugajj na kufuta mashamba 16 yasiyoendelezwa ili yapangiwe matumizi ya kilimo na ufugaji.

Ameyataja maamuzi mengine yaliyofikiwa kwenye kikao hicho cha Baraza la Mawaziri ni kuitaka Ofisi ya Makamu wa Rais, ikamilishe mwongozo utakaobainisha matumizi ya ardhi ndani ya hifadhi ya mita Sitini za mito, vyanzo vya maji, maziwa na bahari.

Maamuzi mengine ni kuzitaka Wizara na taasisi zote za Serikali zilinde maeneo yao kwa kuweka alama za kudumu zinazoonekana na kwamba Wananchi hawaruhusiwi kuvamia maeneo mapya na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya uvamizi wowote kuanzia hii leo.