RC Makonda afanya ukaguzi wa ujenzi wa Stendi ya Mbezi

0
198

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda leo ametembelea na kukagua maendeleo ya Ujenzi wa kituo kipya cha kisasa cha Mabasi yaendayo Mikoani na Nchi za Jirani kilichopo Mbezi Luis ambacho ujenzi wake umefikia asilimi 35 hadi sasa na kumtaka Mkandarasi kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

Makonda amesema ujenzi wa kituo hicho utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 50.9 ambapo ndani yake kutakuwa na huduma zote muhimu ikiwa ni pamoja na Jengo la Abiria,Utawala, Maegesho ya mabasi 500, Maduka Makubwa, Hoteli, Maegesho ya Taxi, Bajaji, Pikipiki, Benki, Vituo vya Mafuta, Nyumba za kuishi, ofisi za mabasi, sehemu ya wafanyabiashara, mama Lishe,Vyoo, Kituo cha Polisi na sehemu ya kuhifadhi mizigo.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es salaam, amemuelekeza Katibu Tawala wa Mkoa huo kuunda Kamati ya kufuatilia Maslahi ya wafanyakazi wote wanaofanya kazi katika miradi ya kimkakati ili kuhakikisha wanapata stahiki zao zote ikiwemo mishahara na kuunganishwa na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Pamoja na hayo RC Makonda ameendelea kuwataka wakandarasi wa miradi mbalimbali kuhakikisha wananunua vifaa kutoka kwenye Viwanda vya ndani jambo litakalosaidia kuinua uchumi wa Viwanda.

Katika Ziara hiyo Makonda ameambatana na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam.