Miili ya waliokufa kwenye ajali ya ndege yasafirishwa

0
172

Miili ya Watu wawili waliokufa baada ya ndege ndogo mali ya kampuni ya Auric Air kuanguka huko wilayani Serengeti mkoani Mara, imesafirishwa na kupelekwa jijini Dar es salaam ili kuendelea na taratibu nyingine.

Akizungumza kwa njia ya simu na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Msemaji wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) Pascal Shelutete amesema kuwa Miili hiyo ni ya Rubani wa ndege hiyo Nelson Mabeyo ambaye ni mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo na mwingine wa Nelson Orutu ambaye ni Rubani Mwanafunzi, ambao wote wawili wamefariki Dunia katika ajali hiyo.

Taarifa ya awali ya ajali hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Thomas Ngulika imeeleza kuwa, ndege hiyo ndogo aina ya C 208B imeanguka majira ya asubuhi hii leo, muda nfupi baada ya kupaa katika kiwanja kidogo cha ndege cha Seronera.

Imesema kuwa, ndege hiyo ilikua ikielekea katika kiwanja kingine cha ndege cha Grumeti kwa ajili ya kupakia abiria, ambapo viwanja vyote hivyo viwili vinamilikiwa na TANAPA na vipo wilayani Serengeti.

Taarifa hiyo ya Mhandisi Ngulika imeeleza kuwa, ndege hiyo imeharibika kabisa kiasi cha kutotumika tena na kwamba Mkaguzi wa ajali za ndege kutoka wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano tayari ametumwa eneo la tukio ili kuandaa taarifa kamili.