Wanafunzi Saba wamefariki Dunia baada ya darasa walilokua wakisomea kuanguka katika shule ya watoto wenye vipaji maalumu ya Precious iliyopo jijini Nairobi nchini Kenya.
Habari kutoka jijini Nairobi zinasema kuwa, darasa hilo liliojengwa kwa kutumia mbao, limeanguka muda mfupi baada ya Wanafunzi kuanza masomo yao hii leo.
Wanafunzi wengine wengi wanadhaniwa kunasa kwenye kifusi na vikosi vya uokoaji vipo katika eneo la tukio na vinaendelea na kazi ya uokoaji.
Hata hivyo waokoaji hao wamesema kuwa kazi ya uokoaji imekua ngumu, kutokana na watu wengi kuzingira eneo la shule hiyo ya watoto wenye vipaji maalum ya Precious, hali inayofanya washindwe kuifanya kazi hiyo vizuri.
Watu waliozingira eneo lilipoanguka darasa hilo wameshutumu zoezi la uokoaji kufanyika taratibu, hali inayoweza kusababisha madhara zaidi.
Chanzo cha darasa hilo kuanguka bado hakijafahamika, lakini Mkurugenzi wa Shule hiyo Moses Ndirangu ameulalamikia ujenzi wa bomba la Maji Taka unaoendelea jirani na shule hiyo kuwa huenda umesababisha kudhoofisha msingi wa jengo la darasa hilo.