Rais John Magufuli ameagiza Mahabusu waliopo katika Magereza mbalimbali kwa makosa ya Uhujumu Uchumi, kama wapo tayari kuomba msamaha na kuzirudisha fedha walizotakatisha, wasikilizwe ndani ya siku Saba kuanzia kesho.
Rais Magufuli ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es salaam, wakati akiwaapisha Viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni akiwemo Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata.
Rais Magufuli amesisitiza kuwa, hayo ni mapendekezo yake na si kwamba anaingilia kazi ya Mhimili mwingine.
Amemweleza Naibu Wakili huyo Mkuu wa Serikali mpya kuwa, anapendekeza kama inawezekana Watuhumiwa hao warejeshe fedha hizo serikalini na kisha waendelee na maisha yao ya kawaida.
Amesema kuwa analazimika kutoa kauli hiyo kwa kuwa anafahamu wapo baadhi ya Watuhumiwa wa makosa hayo ya Uhujumu Uchumi wanayasikitikia makosa yao na wanataka kujisafisha ili kuondokana nayo.