Rais Magufuli akerwa na mwenendo wa uboreshaji eneo la Coco Beach

0
145

Rais John Magufuli ameelezea kukerwa kwake na mwenendo wa makabidhiano na usimamizi wa mradi wa kuboresha eneo la ufukwe wa Coco Beach lililopo Oysterbay jijini Dar es salaam.

Rais Magufuli ameoneshwa kukerwa na namna ambavyo makabidhiano na usimamizi wa uendelezaji wa eneo hilo unavyofanywa na Manispaa ya Kinondoni huku akimnyooshea kidole Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, – Paul Makonda kuhusiana na usimamizi wake wa miradi katika mkoa wake.

Akihutubia Ikulu jijini Dar es salaam, wakati wa hafla ya kuwaapisha Viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, Rais Magufuli ameonesha mashaka juu ya Mkandarasi aliyepewa kazi hiyo na kusema kuwa haoni kama ana uwezo wa kuboresha eneo hilo.

Rais Magufuli pia ameshangazwa na namna ambavyo Manispaa ya Kinondoni inavyopanga kujenga maghorofa katika eneo la Coco Beach kinyume na sheria ya mazingira inayotaka ujenzi wowote kwenye Kingo za bahari na maziwa kufanyika umbali wa Mita Sitini.

Rais Magufuli ameongeza kuwa, ameshangaa kuona ujenzi wa eneo hilo unaingiliana na ujenzi wa Daraja linalopita baharini katika eneo la Coco badala ya kutafutiwa sehemu nyingine.

Aidha Rais Magufuli ametaka kusimamiwa kwa karibu eneo hilo ili fedha za walipa Kodi wanyonge ziweze kuwa na manufaa kwao na Taifa kwa ujumla.

Amewaagiza Watendaji wote wa Serikali kusimamia vizuri fedha za walipa Kodi, ili ziweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa Wananchi na hasa Wanyonge.