Serikali imetangaza utaratibu mpya wa ununuzi wa Korosho, wenye lengo la kuongeza faida kwa Wakulima na kuongeza thamani ya viwanda vinavyobangua korosho hapa nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameutaja utaratibu huo kuwa ni wa kutumia Minada ya wazi itakayoendeshwa Kidigitali, ambapo Mnunuzi ataweza kuifuatilia akiwa katika sehemu yoyote Duniani.
Amesema kuwa msimu wa ununuzi wa Korosho kwa mwaka huu utaanza rasmi Septemba 30, ambapo pia utafanyika mkutano wa Wadau wote wa Korosho kueleza namna ya kujisajili katika Minada ya wazi ya ununuzi wa Korosho hizo.
Waziri Hasunga ameongeza kuwa, kwenye msimu wa mwaka 2018 wa ununuzi wa Korosho, Serikali ilinunua Korosho zote za Wakulima ambazo zilikua na thamani ya Shilingi Bilioni 723 na kuwalipa Wakulima.
Amefafanua kuwa deni lililobaki halizidi Shilingi Bilioni 50, ambalo Serikali inaendelea kuwalipa Wakulima.