Rais John Magufuli amefanya uteuzi wa baadhi ya viongozi ikiwa ni pamoja na Naibu Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa, Mkuu wa mkoa mmoja na Mabalozi mbalimbali watakaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi.
Katika uteuzi huo uliotangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Rais Magufuli amemteua Lowata Sanare ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha kuwa Mkuu wa mkoa wa Morogoro kuchukua nafasi ya Dkt Steven Kebwe.
Katika uteuzi huo, Rais Magufuli pia amemteua Musa Masele ambaye ni Msaidizi wa Mkuu wa mkoa wa Geita kuwa mkuu wa wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro.
Rais Magufuli ameteua Mabalozi 12 ambao wataiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali Duniani, ambapo uteuzi huo unatokana na nafasi hizo kuwa wazi baada ya Mabalozi kumaliza muda wao, Kustaafu ama kurejeshwa nyumbani ambapo watapangiwa kazi nyingine.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), -Modestus Kipilimba, yeye pia ameteuliwa kuwa Balozi na kituo chake cha kazi kitatangazwa baadae.