Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo hazina Bandari, kuitumia bandari ya Dar es salaam kusafirishia mizigo inayotoka na kuingia katika nchi hizo ili kukuza uchumi wa Ukanda huo.
Akifungua mkutano wa Mawaziri wa Mawasiliano ,Uchukuzi, Tehama na Hali ya Hewa unaofanyika jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu Majaliwa amezitaka nchi hizo kuitumia bandari hiyo ambayo kwa sasa imeboresha utoaji huduma.
Amesema kuwa, ukuaji wa uchumi endelevu wa nchi za SADC unategemea utangamano na ushirikiano baina ya nchi hizo na kuzitaka kutumia miundombinu ya Bandari ya Dar es salaam kusafirishia mizigo yao.
Kuhusu ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Ukanda wa SADC, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa maendeleo ya teknolojia yanaweza yakaharakisha ukuaji wa uchumi katika nchi za SADC.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua mkutano huo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa, mkutano huo utatoa mwelekeo wa maendeleo ya sekta ya Mawasiliano, Uchukuzi, Tehama na Hali ya Hewa katika Ukanda wa SADC.