Morogoro yatajwa kukithiri kwa matumizi mabaya ya fedha za umma

0
193

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Morogoro, -Dkt. Steven Kebwe kuuangalia vizuri mkoa huo kwa kuwa umekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Akiwa katika siku ya Tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro, Waziri Mkuu amesema kuwa, akiwa katika ziara hiyo amepata taarifa kuwa zaidi ya Shilingi Milioni Tisa zimetumika kwa ajili ya kulipana posho katika Halmashauri ya Mji Ifakara.

Amemweleza Dkt Kebwe kuwa, posho hizo ni kwa ajili ya ziara ya Waziri Mkuu na imetoka kwa Mtendaji wa Kata ya Viwanja Sitini, jambo ambalo halikubaliki.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa amemkabidhi Mkuu huyo wa mkoa wa Morogoro risiti zote ili awachukulie hatua wote waliohusika na matumizi hayo mabaya ya fedha za umma wakati wa ziara yake.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa Ujenzi wa wilaya ya Morogoro, -Brown Undule baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ikiwemo usimamizi mbovu wa ujenzi wa kituo cha afya Mkuyuni.

Amefikia uamuzi huo, baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho na kueleza kuwa
hajaridhishwa na aina ya milango iliyotumika.

“Milango yote katika jengo hili ingolewe leo leo, huwezi kuweka milango ya hovyo namna hii yaani mtu wa nje anamuona aliyeko ndani, nimesitisha kuendelea kukagua jengo, yeye na usomi wake ameridhishwa na milango ya hovyo kama hii”, amesisitiza Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa, aina ya milango iliyowekwa katika kituo hicho cha afya haiwezi kutumika hata kwenye nyumba ya mtu binafsi, lakini kutokana na uangalizi mbovu kutoka kwa Watendaji wamekubali kuweka milango hiyo.