Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Khalifa Abdulrahman Al -Mazzouqi ametoa fedha kwa ajili ya ufadhili wa masomo ya kidato cha Tano na Sita kwa Wanafunzi 100 wa Kike waliofaulu katika michepuo ya Sayansi.
Akizungumza jijini Dar es salaam katika hafla ya kukabidhi fedha kwa ajili ya ada, sare na mahitaji mengine kwa Wanafunzi hao, Balozi Al- Mazzouqi amesema kuwa ufadhili huo ni mwanzo tu na ofisi yake itaongeza zaidi ufadhili katika miaka ijayo.
Aidha ameongeza kuwa Ubalozi wa Falme za Kiarabu hapa nchini utaendelea kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Dar es salaam katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kuwasaidia Wananchi wa mkoa huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, -Paul Makonda amemshukuru Balozi huyo kwa namna anavyojitoa kusaidia jitihada zake za kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali katika mkoa wake.
Aidha Makonda amesema kuwa, ameamua kusaidia jitihada za Rais John Magufuli katika kuongeza kiwango cha elimu kwa Watanzania wasio na uwezo ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao za kielimu.
Jumla ya Wanafunzi wa Kike Mia Moja waliofaulu masomo ya Sayansi katika mitihani yako ya kidato cha Nne mwaka 2018, wamepatiwa ufadhili wa masomo kupitia mfuko wa Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam wa kusaidia Elimu kwa Wasichana wanaotoka katika familia zisizojiweza, lakini wamefaulu masomo yao ya Sayansi.
