Tume yaundwa kushughulikia miradi ya kimkakati Dar

0
173

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, – Paul Makonda ameunda Tume itakayoongozwa na Katibu Tawala wa mkoa huo Abobakar Kunenge, kushughulikia miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali Kuu katika mkoa huo.

Makonda ametoa taarifa ya kuundwa kwa Tume hiyo wakati akizungumza na Watendaji na Wazazi wa Wanafunzi wa Kike waliopatiwa ufadhili wa kusoma kidato cha Tano baada ya kufaulu masomo yao Sayansi, ufadhili unaotolewa kupitia mfuko ambao ameuanzisha.

Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es salaam ameunda Tume hiyo kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Rais John Magufuli ya kuwataka viongozi wa mkoa wa Dar es salaam kusimamia kwa ukaribu miradi inayotekelezwa na serikali katika mkoa huo.

Akitoa maelekezo hayo, Rais Magufuli alionesha kukerwa na ucheleweshwaji wa mradi wa Machinjio ya Kisasa katika eneo la vingunguti na ule wa uboreshaji wa eneo la Coco Beach.

Baada ya maelekezo hayo ya Rais Magufuli,- Makonda ametangaza kuunda Tume hiyo ambayo itasimamia miradi mnne inayotekelezwa na Serikali Kuu katika mkoa wa Dar es salaam ambayo ni ujenzi wa Soko la Kisutu, Ujenzi wa Machinjio ya kisasa Vingunguti, Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Mbezi na Uboreshaji wa eneo la Coco Beach.