Suala la mtoto kukatwa mkono, wizara ya Afya yavalia njuga

0
195

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee wa Watoto Dkt Faustine Ndugulile amemuagiza Msajili wa Baraza la Madaktari la Tanganyika kushirikiana na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania, kufuatilia suala la mtoto aliyekatwa mkono baada ya kuhamishiwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliyopo jijini Dar es salaam kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala.

Dkt  Ndugulile ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati akizindua bodi ya Nane ya Maabara Binafsi za Afya.

 “Nilitegemea Baraza la Madaktari muwe mmeanza uchunguzi, kwa hiyo nakupa maagizo kesi hiyo muanze kufuatilia na kama itathibitika ni uzembe waliohusika wachukuliwe hatua, ndani ya wiki mbili mtuletee majibu ili mimi na Mheshimiwa Waziri tujue tunachukua hatua gani” amesisitiza Naibu Waziri Ndugulile.

Taarifa za mtoto huyo kukatwa mkono kwa kile kinachodaiwa kuwa ni uzembe wa wahudumu wa afya katika hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala ziliibuliwa Jumamosi iliyopita na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia kipindi chake cha Hadubini.

Amesema kuwa,  kwenye Mabaraza bado kuna changamoto ya baadhi ya mashauri kuchukuliwa hatua,  hivyo kama Mabaraza ya kitaaluma ni vyema kuangalia ufanisi wa majukumu yao na kuchukulia hatua pale taaluma inapokosewa na waliokosea wachukuliwe hatua. 

Dkt. Ndugulile ameitaka bodi  hiyo ya Nane ya Maabara Binafsi za Afya kusimamia usajili wa maabara zote nchini kwa kuwa hivi sasa kumekua na uanzishwaji wa maabara bila kuzingatia sheria.

 “Naomba sheria ifuate mkondo wake ili kubaini wale wote walioanzisha huduma za maabara bila kufuata sheria na taratibu za usajili, tushirikiane kuhakikisha kuwa hakuna taasisi au mtu atakayefungua au kutoa huduma za maabara bila kusajiliwa”, amesisitiza Dkt Ndugulile.