Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu kuanza kesho

0
1039

Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara unaanza kuunguruma rasmi hapo kesho kwa michezo kadhaa kuchezwa kwenye viwanja tofauti.

Bingwa mtetezi Simba atakuwa na kibarua kizito mbele ya wakata miwa wa Mtibwa kwenye mchezo utakaochezwa katika dimba la Uhuru jijini Dar es salaam kuanzia majira ya saa Kumi alasiri.

Simba itashuka dimbani bila ya huduma ya mshambuliaji wake John Bocco ambaye bado hajawa fiti kwa asilimia Mia Moja na tayari kocha wa timu hiyo Patrick Aussems amesema kuwa, atalazimika kumtumia Meddie Kagere ambaye alikuwa na majukumu ya Kimataifa Jumatatu hii kwani hana chaguo lingine.

Mchezo mwingine hapo kesho utakuwa kati ya wenyeji Coastal Union watakaokua nyumbani kwenye dimba la Mkwakwani jijini Tanga kuwakaribisha KMC ya Dar es salaam.

Kwa mujibu wa tovuti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Keshokutwa Jumamosi itachezwa michezo Mitatu, ambapo Namungo watakuwa nyumbani kuwaalika Singida United wakati JKT Tanzania watamenyana na Lipuli huku Mbao FC wakiwakaribisha Biashara United ya Mara.