Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Mamlaka za maji kote nchini, kuacha mara moja kupandisha bei za maji kwa kigezo cha kufidia gharama za ujenzi wa miradi ya maji, kwa kuwa miradi hiyo imegharimiwa na serikali ili Wananchi wapate huduma hiyo kwa bei nafuu.
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu Majaliwa ameitoa Bungeni jijini Dodoma, wakati wa kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu ambapo alikua akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Mariam Kisangi.
https://www.youtube.com/watch?v=aVLviA-WZbM&feature=youtu.be
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Serikali haikubaliani na hatua zinazochukuliwa na mamlaka nyingi za maji kupandisha bei ya maji kwa kigezo cha kufidia gharama za miradi hiyo ya maji.
Waziri Mkuu ameiagiza wizara ya Maji, kuhakikisha inashughulikia tatizo hilo ambalo limekuwa kero kwa Wananchi na kulipatia ufumbuzi wa haraka, ili lisiendelee kuwaumiza Wananchi.
“Haiwezekani bei za maji kupanda kutoka Shilingib Elfu Tano hadi kufikia Shilingi Elfu 28 kwa mara moja, hii ni kuwaumiza Wananchi na sisi kama serikali tunasema haiwezekani”, amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuboresha huduma za maji na kamwe haitakubali kuona gharama za maji zikiendelea kuwa kubwa.
Kwa upande wake Spika wa Bunge,- Job Ndugai ameitaka Serikali kuhakikisha inasimamia gharama za maji kwa kuwa kumekuwa na upandaji holela wa bei za maji na hivyo kuwaumiza watumiaji wa huduma hiyo.
