Nape aomba radhi kwa Rais Magufuli

0
178

Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, – Nape Nnauye, leo amekutana na kumuomba radhi Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, kufuatia kuhusika kwake katika mazungumzo yasiyofaa dhidi ya Rais Magufuli.

Baada ya mazungumzo hayo, yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Nape amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali ombi lake la kukutana nae na kumsikiliza, na pia kumsamehe kwa makosa aliyoyafanya kufuatia taharuki iliyoibuka baada ya kuvuja kwa sauti za mawasiliano yake na Wanasiasa wengine wakimsema Rais Magufuli.

“Kwa hiyo baada ya kupata fursa nimekuja nimemuona, na mle ambamo nilimkosea kama Baba yangu nimeongea nae na Baba amenielewa, ameniambia amenisamehe na amenipa ushauri ambao nitaufanyia kazi na naamini baada ya hapa mambo yatakwenda vizuri, na kwa kweli kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru sana sana, amenipa fursa kubwa, ndefu na ameongea maneno mengi kwangu na ushauri wake nimeuchukua” amesema Nape Nnauye.

Kuhusu maendeleo, Nape amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali na amesema ana matumaini kuwa CCM itapata ushindi katika chaguzi kutokana na kazi hiyo.

Kwa upande wake, Rais Magufuli amesema kuwa Nape amekuwa akiomba kukutana nae mara nyingi na tangu siku nyingi kupitia kwa watu mbalimbali wakiwemo Wasaidizi wake, viongozi Wastaafu na viongozi wa CCM na kwamba baada ya kukutana nae na kumuomba radhi ameamua kumsahehe.

Rais Magufuli amemtaka Nape kwenda kufanya kazi za kuhudumia wananchi wa Jimbo lake la Mtama na kukitumikia vyema chama chake cha CCM.


“Yote nimesamehe, huyu bado ni kijana mdogo, ana matarajio makubwa katika maisha yake, mimi nikiendelea kumshikilia kwenye moyo wangu kwanza ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu na tumefundishwa katika maandiko yote tusamehe Saba mara Sabini, kwa hiyo nimemsamehe na Mungu amsaidie katika shughuli zake akafanye kazi zake vizuri, akalee Mke wake na familia yake, akakitumikie chama, akawatumikie wananchi wa Jimbo lake vizuri, mimi nimemsamehe, labda kama yeye atakengeuka hiyo itakuwa ni juu yake, lakini mimi kutoka moyoni mwangu nimeshamsamehe na nimemsaheme kweli, Nape nenda ukafanye kazi, Mungu akujaalie” amesisitiza Rais Magufuli.