Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amezindua huduma ya ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa kutumia mtandao wa simu ya mkononi kupitia Airtel Money.
Kupitia huduma hiyo, Wamiliki wa ardhi wataweza kufanya malipo kupitia mtandao huo wa simu bila kwenda ofisi za ardhi.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa akizindua huduma hiyo, Waziri Lukuvi amesema kuwa ubunifu wa serikali kufanya malipo ya ankara za serikali kwa kutumia mfumo wa GePG umerahisisha malipo ya tozo mbalimbali ikiwemo kodi ya pango la ardhi.
Amesema kuwa, mfumo huo wa malipo ya serikali umekuja na faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuweka kumbukumbu vizuri, kulipa kwa muda, kupunguza upotevu wa mapato ya serikali, kuondoa mianya ya rushwa pamoja na kuongeza mapato ya serikali.
‘’Tunayo furaha kubwa kwa mara nyingine kutangaza kuwa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel imerahisisha malipo ya kodi ya pango la ardhi kupitia Airtel Money, hii ni huduma rahisi na itapunguza kero nyingi wakati wa kufanya malipo’,’ amesema Waziri Lukuvi.
Waziri Lukuvi ameitaka kampuni hiyo ya simu za mkononi ya Airel, kuhimiza Wananchi wanaotumia mtandao wa simu wa kampuni hiyo kulipia tozo mbalimbali za serikali, ikiwemo kodi ya pango la ardhi kwa airtel money kwa kuwa inarahisisha kufanya malipo mahali popote.
Waziri Lukuvi amesema lengo la wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa sasa, ni kutaka kutumia kampuni za simu kuwakumbusha wananchi kulipia kodi ya pango la ardhi kupitia jumbe za simu badala ya utaratibu uliopo sasa wa kuwafuata wadaiwa.