29 wauawa katika mashambulio Burkina Faso

0
504

Watu 29 wameuawa katika mashambulio mawili tofauti nchini Burkina Faso, mashambulio yanayodaiwa kufanywa na Wanamgambo.

Habari kutoka nchini humo zinaeleza kuwa, watu 15 wameuawa baada ya lori walilokua wakisafiria kukanyaga bomu linalodaiwa kutengenezwa kienyeji katika jimbo la Sanmatenga, na kisha lori hilo kulipuka.

Maafisa wa Polisi katika jimbo hilo wamesema kuwa, wengi wa watu waliouawa katika tukio hilo, ni Wafanyabiashara.

Watu wengine 14 wameuawa baada ya Wanamgambo hao kuushambulia msafara uliobeba chakula kilichotolewa na Shirika la Mpango wa Chakuka Duniani(WFP) kwa ajili ya watu walioathiriwa na mapigano.

Zaidi ya watu Mia Tano wameuawa katika mashambulio yaliyofanywa na Wanamgambo hao nchini Burkina Faso kuanzia mwaka 2015 hadi hivi sasa.

Mengi ya mashambulio hayo yamekua yakitokea katika eneo la Kaskazini na Mashariki la nchi hiyo, maeneo yanayopakana na nchi za Mali na Niger.