Serikali kufuatilia mifumo ya huduma za kifedha ili iwe rafiki kwa Wenye ulemavu

0
148

Serikali imesema kuwa inaendelea kufuatilia huduma zinazotolewa na Taasisi za fedha nchini ili ziweze kuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu na hasa mashine za kutolea fedha ATM.

Naibu waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji ametoa taarifa hiyo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Amina Moleli aliyetaka kujua ni lini serikali itaweka mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu kuzifikia huduma za kifedha kwa urahisi.

https://www.youtube.com/watch?v=7bb6_bVn3OI

Akijibu swali hilo, Dkt Kijaji amesema kuwa, mifumo ya mashine za ATM bado sio wezeshi kwa watu wenye ulemavu na kuahidi kuwa serikali inaendelea kuzisisitiza Benki kuweka miundombinu itakayokuwa rafiki kwa watu wa aina hiyo.

Ameongeza kuwa, hadi sasa hakuna ATM inayoweza kuhudumia watu wenye ulemavu wa macho kutokana na changamoto ya teknolojia, lakini serikali inaendelea na mazungumzo na benki ili watu wenye tatizo la kuona waweze kupata huduma hizo kwa urahisi.

Katika swali lake la nyongeza Mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto ameuliza namna serikali inavyoweza kuwasaidia watu wenye ulemavu wa vidole kupata huduma ikiwa hawataweza kujisajili kwa kutumia alama za vidole.

Naibu Waziri Dkt Kijaji amesema kuwa wizara ya Fedha na Mipango itashirikiana na wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha wanatafuta njia mbadala itakayowezesha watu wenye changamoto za ulemavu kuendelea kupata huduma mbalimbali.