Rais John Magufuli amemuelezea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa alikuwa ni Mzalendo wa kweli aliyeipenda Afrika na ndio maana alishiriki katika ukombozi wa nchi nyingi za Bara hilo.
Akihutubia wakati wa uzinduzi wa jengo la Taasisi ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amesema kuwa wakati wa uhai wake Mwalimu Nyerere alipinga ubaguzi na ukoloni katika Bara zima la Afrika.
Katika Hotuba hiyo Rais Magufuli amesema kuwa, mara nyingi Nabii amekuwa hakubaliki nyumbani lakini kwa Mwalimu Nyerere ilikua tofauti, na mara zote amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha ukoloni unakwisha kabisa ndani ya Bara la Afrika.
Aidha Rais Magufuli amemsifu Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwa kuendelea kumuenzi Hayati Baba wa Taifa kila mwaka ambapo nchini Uganda hufanyika Misa maalumu ya kumuombea Hayati Baba wa Taifa.
Kwa upande wake Rais Museveni amesema kuwa, katika uhai wake Mwalimu Nyerere alifaulu katika kila Nyanja kuanzia diplomasia, uchumi, siasa, utamaduni na hata kuhasisha umoja wa Taifa la Tanzania.
Rais Museveni amewataka Waafrika kuendelea kumuenzi Hayati Mwalimu Nyerere kwa kuwa jitihada zake ziliwezesha Bara la Afrika kujikomboa kutoka katika utalawa wa Kikoloni.